×
×

MTAALAMU WA UREMBO NA MWENYE MOYO WA UFADHILI

Flora Lauo ni mfano halisi wa urembo wa ndani na nje

Na Theresia Christian

Swahili English

Sikumfahamu Flora nilipomwita kwa ajili ya mahojiano.

Baada ya kuwasiliana kupitia simu alianza kuniita “mpendwa” kama mama mpendwa mwenye upendo wa kweli. 

Na hivyo ndivyo alivyonitendea tulipokutana kwa mara ya kwanza. Alinikaribisha kwa tabasamu kubwa na sauti yake ya kunikaribisha iliyonikumbatia sawa na shuka zito—sawa tu anavyowatendea watoto wake wanaomwita kwa jina la ‘Mama.’

Flora, ni mwanamke kijana mrefu na ameolewa na kupata watoto wawili. Hata hivyo, yeye pia ni mwanzilishi wa kituoo cha NIFO Hope Center, kinacholea watoto wanaoishi katika mazingira magumu—wengi wao wameteseka kwa kunyanyaswa kingono au kimwili—na kuwapatia usalama mbali na masaibu ya dunia. Wazo la kuanzisha kituo hivyo lilimjia alipotembelea na kukutana na watoto waliokuwa na utapiamlo na maskini wa ji wa nyumbani kwao wa Marangu, Kilimanjaro, na akachochewa kuwachukua na kuwatunza ili wasipatwe na kifo.

“Nilianza na mtoto mmoja,” anakumbuka, “kisha wa pili, watatu…mwishowe nikagundua nina watoto nane wanaishi nyumbani kwangu. Mwanzoni mume wangu aliniambia, ‘Unataka kufanya nyumba yangu kituo cha kulelea watoto?’” Anakumbuka huku akitabasamu.

Kadiri Flora alivyozidi kuleta watoto zaidi nyumbani kwake ndivyo alivyogundua mahitaji na changamoto zao. 

“Baadhi yao wakujua hata kuongea Kiswahili; wengine walikuwa hawajui hata jinsi ya kutumia maliwato. Wengine walivunja vitu nyumbani kwangu, wakachana viti—na walifanya mambo mengine ambayo kama huna moyo wa kusaidia viumbe hao wadogo, huwezi kukaa nao hata juma moja na hata watano wao,” akasema. “Hata hivyo niliwavumilia na niliwapenda.”

Subira yake na upendo wake wa dhati ulikuwa na matokeo mazuri japokuwa mwanzoni hali ilikuwa ngumu. Flora alilelewa katika familia iliyokuwa na hali ngumu kiuchumi hivi kwamba ilimlazimu aache kuendelea na masomo yake ya sekondari. Baada ya kuacha alianza kufanya kazi ya kutengeneza nywele ili kujiruzuku na akaamua kufanya mengi zaidi katika fani hiyo baada ya saluni yake kuibiwa na kukumbwa na mafuriko. 

Leo ana biashara inayomsaidia kuendesha shughuli nyingi kutia ndani kituo cha Hope Center. Mbali na kituo cha Hope Center, huendesha pia Chuo cha Urembo kinachowasaidia vijana kutoka katika kituo chake kupata ujuzi wa kufanya biashara ya urembo. Malengo yake ni kuwawezesha vijana kutimiza ndoto zao bila kujali wamelelewa katika hali gani. 

Kituo cha Hope Center, kimepata mafanikio makubwa tangu kilipofunguliwa. Kilianza kukua baada ya kukosekana kwa nafasi: kufikia wakati huo watoto 16 walikuwa wakiishi katika nyumba ya vyumba vitatu ya Flora, na alikuja kujua kwamba ni kinyume cha sheria kuishi na idadi hiyo ya watoto bila kufuata taratibu za kisheria. Hivi sasa, kituo cha Hope Center kinatunza watoto na vijana 60 ingawa idadi hiyo hubadilika. 

Baadhi ya watoto huishi hapo kwa kipindi kifupi ikitegemea na kwa kipindi gani kitachukua mpaka walezi watajitokeza wa kulea watoto hao. “Baada ya hapo, ikiwa ndugu wa mtoto wataonyesha nia ya kutaka kuwalea, basi kituo hufuatilia maendeleo ya mtoto huyo katika nyumba atakayoishi.,”anafafanua Flora. 

Kuna watoto wengine ni wakazi wa kudumu katika Kituo kwa kuwa ni yatima au hali mbaya nyumbani kwao. Kwa watoto ambao ni wahanga wa kunyanyaswa kijinsia au kimwili, ni vigumu sana kwa Flora kuwaruhusu watoto hao kurudi ili kuishi na familia zao.

Macho yake hujaa huzuni anapokumbuka masimulizi ya watoto hao waliokabili manyanyaso hayo. “Kwa mfano, mtoto mmoja alibakwa na mjomba wake alipokuwa na umri wa miaka mitatu. Kwa sababu hiyo mfuko wake wa uzazi uliondolewa. Ni mtoto mrembo sana lakini kwa sababu ya hali yake hataweza tena kupata mtoto wake [siku moja],” anasema. “Siwezi kumrudisha msichana huyu nyumbani kwao …kesi yake bado iko mahakamani,” anasema.

Kukataa kwake kuwarudisha watoto hao nyumbani kutoka na kuwa na hali mbaya nyumbani huko kumewasaidia sana watoto hao kuwa salama. Hata hivyo, hali hiyo imepelekea Flora kutishiwa maisha yake. “Baadhi ya watu huniona mimi kuwa adui. Maisha yangu yako hatarini kwa sababu ninajali,” anasikitika. “Hata ninapoendesha gari, inabidi nihakikishe kwamba nimefunga madirisha.” Anaanza kulia. “Sasa sina furaha asilimia 100,” anasema. “Kuna matukio yaliyonifanya nihofu usalama wa maisha yangu. Pindi moja nakumbuka kuna watu walitumwa kunimwagia tindikali. Hata hivyo nilibahatika; polisi walisaidia kuzuia shambulio hilo.” Aacha kuongea ili kufuta machozi yake. 

Matukio hayo mabaya si mambo ya kuchukulia kivivi hivi tu. Mbali na kutishiwa maisha yake, si rahisi kwa Flora kuruzuku familia yake. “Kuna wakati sijui watoto watakula nini kesho kwa sababu sina pesa ya kutosha kuwanunulia chakula,”anakiri. “Ninahisi vibaya sana, mimi hutoa machozi tu. Hata hivyo hupata ujasiri na kuomba msaada wa watu na ninamshukuru Mungu kwani wengi wao hunisaidia.” Michango hiyo ya watu mmoja mmoja ndiyo inayoendesha Kituo hiki, na Flora anaamini wataendelea kuchangia Kituo bila kusita. 

Bila kujali kitakachotokea wakati ujao, Flora amejizatiti kuendelea kusaidia watoto waliogusa moyo wake. 

“Mimi hufurahia sana kuwasaidia watoto hawa,” anasema. “Pindi nyingine mimi huenda nyumbani usiku kwa sababu baadhi ya watoto waliniomba niwe nao mpaka wanapopitiwa na usingizi kitandani. Basi mimi husubiri mpaka wanapolala kisha huondoka … Mimi hutumia wakati wangu mwingi Kituoni,” anasema.

Anapotazama wakati ujao, Flora huonyesha shangwe yake na mtazamo chanya kuhusu maisha anaopata kila mara anapokuwa na watoto wake. Akiwa anaendesha Kituo cha Hope Center, Chuo cha Urembo, na biashara nyingine , tayari ana moyo mzuri—upendo wa dhati—vitu tosha kukabiliana na lolote wakati ujao. 

Maelezo Kuhusu Mwandishi

Theresia Christian

Theresia Christian:

Hi, am Theresia Christian, a mother, an academic at the St. Augustine University of Tanzania. Am also a small business owner. I am passionate about writing and reading, inspiring and learning from others. I am also part of Dreamlink team in Mwanza. Am just excited and glad to join this amazing platform..

1
MAONI Sambaza

0 Maoni

Ili uandike maoni katika DreamLink ni lazima uwe umejisajili na umeingia katika akaunti. Tungependa kupata maoni yako hivyo acha tukusajili sasa!

Ingia