×
×

KUFUNGUA NIJA KUTOKA JANGA MPAKA KUWA NA UHURU

Aiysha akomesha kasumba kwa kuwa  mwanamke wa kwanza kutembeza watalii Zanzibar

Na Ayushi Ramaiya

Swahili English

Watembeza watalii karibu watano hivi walinifuata nilipokuwa nimekaa katika Bustani ya Forohani ya Zanzibar, eneo la Stone Town lenye idadi kubwa ya watu wanaofanya mazoezi kwa kukimbia na watalii. 

Watembeza watalii hao ambao wote walikuwa wanaume, hawakusita kutangaza huduma wanazotoa. Hata hivyo, nilikataa huduma zao kwa kuwa nilikuwa natarajia kutembezwa na mtu mmoja aliyekuwa tofauti sana na wao. 

Kisha kwa mbali nikamwona Aiysha akija. Alikuwa amevalia gauni, kichwani amevaa ushungi wa rangi nyekundu na akiwa na tabasamu bashasha. Kwa mtu asiyemfahamu anaweza akafikiri ni mwanamke akiwa matembezini katika eneo la bustani. Hata hivyo nilimtambua kulingana na wasifu wake: mwanamke wa kwanza mtembeza watalii Zanzibar. 

Kama tukio eneo tulilopanga kukutana na Aiysha ndilo eneo ambalo miaka 10 iliyopita alifanya kwa mara ya kwanza kazi ya kutembeza watalii. Mteja wake wa kwanza alikuwa mwanamke aliyetaka kufahamu mji vizuri. “Sina pesa ya kukulipa,” alimwambia Aiysha. 

Hilo halikuwa jambo la muhimu kwa Aiysha pindi hiyo. “Nikasema, ‘Hakuna shida,’ na mara moja nikajitambulisha kwake kama mtembeza watalii,” anakumbuka. “Siku iliyofuata nilimtembeza na mfukoni alikuwa na dola mbili za marekani, [lakini] akaniambia angenifundisha mbinu mpya za kutangaza biashara.” Akaendelea kusema, “Tulianza matembezi katika Bustani za Forodhani na mtalii huyo akanikaribisha chakula, ila mimi nilikuwa na njaa na kiu ya ujuzi..”

Safari yake ya kwanza ingawa ilikuwa ya ghafla, ilikuwa jambo kubwa katika kazi ya Aiysha ya kutembeza wageni. Elimu ya biashara aliyojifunza kutoka kwa mteja ilimsaidia kuboresha mbinu za kutangaza biashara yake na kupata wateja, jambo lililomsaidia kupata mafanikio katika kazi yake ya kutembeza wageni. 

Leo, Aiysha hatembei mitaani kutafuta wateja wa kuwatembeza kama watu wengine wanavyofanya. Anatumia muda wake mwingine kuandika au kujibu barua-pepe au jumbe kwenye mitandao ya kijamii ambamo wateja wake wanaotaka  huduma ya kutembezwa hutuma. Haikuchukua muda mrefu kugundua kwamba kuna uhitaji mkubwa wa watembeza watalii wa kike wa kujitegemea.

Hata hivyo kumbuka kwamba maisha mazuri anayoishi sasa na biashara nzuri anayofanya Aiysha haikuja kwa bahati tu. Amefanikiwa kwa sababu ya tamaa yake ya kujifunza zaidi—sifa muhimu iliyomsaidia kuendelea kufanya vema mambo yalipokuwa magumu mwanzo mwa maisha yake. 

Alipokuwa mtoto,  Aiysha hakuwa na baba au mama wa kumlea. Baada ya wazazi wake kutalikiana alipokuwa na umri wa miaka mitatu, Aiysha alilazimika kupambana na maisha peke yake. Mama yake aliwakimbia na “baba alifariki nilipokuwa bado nasoma shule ya msingi,” akasema. “Maisha yalikuwa magumu sana nilipokuwa naishi na bibi yangu na nililazimika kufanya kila kitu peke yangu.”

Alipokuwa anasoma shule ya sekondari alijifunza kwa bidii lugha ya Kiingereza na kuweza kuongea kwa ufasaha lugha hiyo, jambo lililomsaidia sana kupunguza mawazo ya matatizo aliyokuwa akikabili na kuweka msingi wa kufanya kazi yake ya kutembeza watalii. 

Alipoamua kusomea utalii katika chuo kikuu aliweka lengo la kufanya vema katika masomo yake. Mwaka wake wa mwisho shuleni, alikuwa mwanamke pekee katika darasa lake. “Rafiki zangu wengi waliachana na masomo na kuanza kufanya kazi katika makampuni ya utalii na kazi yao ilikuwa kuchukua na kuwapeleka wageni uwanja wa ndege,” anakumbuka. Hata hivyo, Aiysha alijua kwamba yeye anataka kufanya mambo makubwa na bora zaidi. “Tangu nilipokuwa mdogo, akili yangu imezoezwa kufanya kazi ngumu na kufuatilia na kutimiza ndogo zangu ili kufanikiwa,” akaongezea.

Haikuwa rahisi kutimiza ndoto zake. Alipohitimu masomo yake ya chuo, alianza kufanya kazi kama mpishi wa familia ya watu kutoka Oman waliokuwa wakiishi Zanzibar. Familia hiyo ilimsaidia kwa kumlipia ada ya kusoma zaidi jambo lililomsaidia Aiysha kuboresha Kiingereza chake na kupata elimu ya kompyuta.

Pia Aalifunga ndoa na kupata watoto wawili ambao walimlazimu kugawa wakati wake wa kazi na familia yake. Wakati huo pia aliutumia kuanzisha uhusiano na mama yake mzazi. 

Jambo la kusikitisha ni kwamba mama na mume wake hawakufurahia kuona Aiysha akijitahidi kutimiza ndoto zake. Kasumba ya kutowathamini wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya utalii ilifanya kuwe na kutoelewana katika familia yake, jambo lililokuwa wazi na kuchangiwa na kipato kidogo cha mume wake. 

“Pindi nyingine tulikunywa uji tu siku nzima,” anakumbuka. “Nilisisitiza na kumwomba aniruhusu kufanya kazi ili kuongeza kipato cha familia. Miaka hiyo miwili ya mwanzo katika ndoa yetu ilikuwa migumu sana.” Ile familia ya Oman ilipompa nafasi ya kufanya nao kazi jijini Muscat, Aiysha alikubali na kwa mara ya kwanza akajionea faida za kusafiri. Hata hivyo wakati huo alikuwa njia panda, anasema “ilibidi nichague moja, kuendelea na ndoa iliyo na matatizo au kupata uhuru wangu.” 

Ingawa mama yake alipinga, alirudi Zanzibar na kuomba talaka. Kufikia wakati huo hakujua maisha yatakuwaje lakini Aiysha hakuwahi kujutia uamuzi wake. Ingawa alianza maisha upya kwa kupanga chumba katika eneo lisilofaa sana na pindi kwa pindi hakuweza kula mlo kamili kwa sababu ya kipato kidogo, aliendelea kuwa na furaha. “Nilihisi kwamba nilishatua mzigo mzito,” akasema.

Aiysha alizidi kuimarika na kufurahia uhuru wake tofauti na matarajio ya wengi. Mwishowe akaamua kujaribu karata yake, akiwafuata watembeza wageni wa kiume katika mitaa ili kuona jinsi wanavyoanzisha mazungumzo na watalii. Mwanzoni hakufanikiwa ingawa alijitahidi sana kuzungumza na watalii. Kwa siku angekutana na watalii kumi lakini labda mmoja angejaribu kuongea naye. Hali hiyo haikumkatisha tamaa Aiysha. Kisha, siku moja akapata mteja wake kwa mara ya kwanza tuliyemtaja mwanzoni.

Baada ya kumtembeza mgeni huyo, watu wengi wakaanza kusikia habari kumhusu Aiysha na siku moja alihojiwa na mwanahabari kutoka Nigeria. Hapo ndipo mambo yalipobadilika na kuwa bora zaidi. “Tangu wakati huo sijawahi kuangalia nyuma,” anasema huku akitabasamu. “Ninapenda kufanya utalii Zanzibar kuwa salama na wenye kufurahisha kwa wanawake na watalii wote kwa ujumla.”

Kama alivyoahidi kutoangalia nyuma, Aiysha anatarajia kutumia vema nafasi za kujiendeleza kimaisha. Hivi karibuni ameanzisha biashara ya nguo ambayo anatarajia itamsaidia kuongeza kipato na kuwaajiri wanawake wengi zaidi na kuwasaidia kuwa na nia ya kufanya ujasiriamali.

“Sitaki kuonwa na wanawake kuwa shujaa,” akasema. “Lakini kwa kuwa nimekabili changamoto nyingi sana, ningependa kuwaongoza wanawake, kuwafundisha kujitegemea na kuwa na furaha kama mimi.”

Ni wazi kwamba Aiysha ni kiongozi iwe anatembeza watalii au anawasaidia wanawake wengine kutambua uwezo wao wa kujiendeleza. Katika sekta yenye mashindano na iliyojaa wanaume, mwanamke aliyevaa nguo ya rangi nyekundu lazima atatambuliwa kwa urahisi. 

Maelezo Kuhusu Mwandishi

Ayushi Ramaiya

Ayushi Ramaiya:

Hi! I am Ayushi, a journalist based in Dar es Salaam. I am an advocate of social change and positive media. My dream is to own a travel channel.

0
MAONI Sambaza

0 Maoni

Ili uandike maoni katika DreamLink ni lazima uwe umejisajili na umeingia katika akaunti. Tungependa kupata maoni yako hivyo acha tukusajili sasa!

Ingia