×
×

AHITIMU TOFAUTI NA MATARAJIO YA WENGI

Sayyeda athibitisha kwamba hakuna kuchelewa katika kutimiza malengo yako

Na Beatrice Bukhay

sayyeda-sons
Swahili English

Elimu haina mwisho.

Wewe muulize Sayyeda, ambaye hivi karibuni alihitimu masomo ya Ufamasia katika  Chuo Kikuu cha Bugando. Mama mwenye watoto wawili alifanya vizuri katika masomo yake huku akifanya kazi na kulea watoto wake, Ali na Ejaz. 

Hakuhitaji kupeleka watoto wake darasani alipokuwa anasoma au kuwalipia shule ya kulea watoto. Hakufanya hivyo kwa kuwa Sayyeda hakupata elimu ya chuo kikuu alipokuwa kijana—alisoma masomo hayo alipokuwa na umri wa miaka arobaini na tatu, umri karibu mara mbili wa wanafunzi wenzake!   

“Katika darasa letu, nilkuwa nasoma na wanafunzi waliokuwa na umri sawa na vijana wangu,” Sayyeda anakumbuka. “Wengi wao waliwaza, ‘Huyu mama mzee anafanya nini darasani kwetu?’”

Si wanafunzi wenzake tu waliojiuliza maswali hayo. Sayyeda anasema kwamba alipoanza masomo yake ya chuo kikuu, ndugu zake na watu wengine walimuuliza maswali mengi, na kuna pindi alitaka kukata tamaa. Hata hivyo, alivyovumilia na kuendelea na nia yake ya kutimiza ndoto yake. Baada ya vikwazo kadhaa mwanzo mwa maisha yake, Sayyeda alijizatiti kutimiza malengo na ndoto zake zilizokatizwa. Kwa kufanya hivyo alibadilisha maisha yake.

sayyeda-portrait

Katika kipindi cha miaka 14 ya ndoa yake, Sayyeda alikuwa mama wa watoto wawili wa kiume na alifanya kazi ya ualimu. Kisha mambo yakabadilika alipotalikiana na mume wake mwaka wa 2009.

“Maisha yalikuwa magumu sana.Nilihisi sina jambo la kufanya au kutegemea,” anatikisa kichwa chake. Ingawa wazazi wake walimruhusu kuishi nao, “kila mtu alipiga porojo kunihusu na watu wa jumuiya yetu walinidharau sana,” anakumbuka. “Wakati huo ulikuwa mgumu sana kwangu na kwa wazazi wangu.” Ingawa anakumbuka machungu hayo, alitulia kidogo na kisha kunywa kinywaji chake na kutabasamu.

Sayyeda hakujua kwamba angepata mafanikio makubwa siku za usoni. Kila kitu kilibadilika alipomsindikiza rafiki yake kwenda CUHAS (Chuo Kikuu cha Bugando), ambapo rafiki yake alitaka kuanza masomo yake ya shahada ya udaktari. Rafiki yake alipokuwa anajisajili, mtu mmoja alimuuliza Sayyeda, “Kwa nini usijiunge na masomo pia?” 

Kabla ya wakati huo, Sayyeda hakuwahi kufikiria jambo hilo. Hata hivyo swali hilo lilipandikiza mbegu ya matumaini katika moyo wake na akaamua kuchukua fomu ya kujiunga. Baada ya kusikia habari hizo, baba yake alimtia moyo kutimiza ndoto zake kwa kujiunga na kozi hiyo. 

“Baba yangu aliniunga mkono kwa kiasi kikubwa sana,” anasea Sayyeda. Basi, “nikajipa moyo na kuchukua fomu na kuanza masomo kama mwanafunzi wa Stashahada ya Madawa mwaka wa 2010,” anaongeza huku akicheka kwa mara ya kwanza tangu tulipoanza mazungumzo yetu. 

Ukizangatia kwamba ni miaka 15 ilikuwa imepita tangu alipokuwa shuleni, Sayyeda alikabili changamoto na kutojiamini kwingi alipokuwa anasoma. Hata hivyo aliamua kukazia fikira masomo yake na kutoruhsu tofauti ya umri kutozuia kutimiza malengo yake. Umakini wake ulimsaidia sana: ijapokuwa alihitaji kufanya kazi ili kuruzuku familia yake na wakati uleule kulipia ada ya shule, Sayyeda alipewa tuzo ya Makamu wa Chuo miaka yote mitatu aliyokuwa shuleni. 

Baada ya kumaliza masomo yake ya Stashahada, chuo kilimpa kazi ya kuwa Mwalimu Msaidizi wa Chuo Kikuu cha CUHAS, kazi iliyomchochea zaidi kuomba kusomea Shahada ya Madawa katika chuo hicho mwaka wa 2014. 

sayyeda-graduating

“Sikutaka kupoteza muda kwa sababu ya umri wangu. Wakati huo nilikuwa nasoma pamoja na mtoto wangu aliyekuwa anasomea udaktari chuo hicho hicho,” anasema huku akitabasamu anapomtazama Ejaz.

Hata hivyo changamoto bado zilimwandamana Sayyeda. Alilazimika kuacha kazi yake na kutegemea mkopo kutoka kwa jumuiya yake ili kuendelea kulipia masomo yake—“ninawashukuru sana kwa msaada wao,” anasema. 

Aliendelea na ushupavu huo mpaka alipohitimu masomo yake na “Nilifaulu masomo yangu yote na kuhitimu mwaka huu,” anasema Sayyeda. Anakunja mikono yake na kufunga macho huku akisali kwa kifupi. 

Ali na Ejaz wanajivunia sana mafanikio ya mama yao. “Tunajivunia kumwita mama yetu. Bidii yake na kupambana kwake ni jambo la kupongeza,” wanasema. “Anatuchochea kuwa watoto na watu bora siku zote.”

Kwa kuwa sasa ana shahada, Sayyeda anataka kujiendeleza hata zaidi.  

“Maisha hutupa njia mbili za kufuata tunapopata matatizo: ama kukaa chini na kulia, au kusimama na kubadili hali,” anashauri. “Nilipoamua kubadili maisha yangu na kuachana na kuhisi vibaya au kujionea huruma, niliweza kuwa na mtazamo mzuri kuhusu maisha yangu—na leo si unaona nilipofika!” 

Hata wanawake wenye moyo mgumu bado wanahisia, machozi yamejaa katika macho ya Sayyeda. Yalikuwa machozi ya shangwe na ushindi na ushindi wa uwezo wake wa kutimiza ndoto zake bila kuruhusu vikwazo vimzuie. 

Maelezo Kuhusu Mwandishi

beatricebukhay@gmail.com

Beatrice Bukhay:

Hello! My name is Beatrice, a Sociologist by profession, a mother, and a small-business owner who is daring to dream big. ⠀⠀⠀⠀⠀⠀⠀⠀⠀ My passion is to work for the community. I have spent three years working in the villages meeting a lot of people especially women who were struggling to make their lives better. It was a good experience seeing very ordinary women having big dreams to change their situations, regardless of all the odds. This taught me that no matter how difficult a situation is, and how unsupportive the environment around you is, if you decide to work on your goals you can change everything and achieve your dreams. ⠀⠀⠀⠀⠀⠀⠀⠀⠀ Being a part of DreamLink is a great opportunity to learn new things and to meet amazing women out there who are daring to dream big, and bring their stories to the forefront to inspire and motivate the readers. ⠀⠀⠀⠀⠀⠀⠀⠀⠀ So, let’s join hands and pledge to turn our dreams into the best reality!

0
MAONI Sambaza

0 Maoni

Ili uandike maoni katika DreamLink ni lazima uwe umejisajili na umeingia katika akaunti. Tungependa kupata maoni yako hivyo acha tukusajili sasa!

Ingia